Aga Khan, Kiongozi wa 49 wa Waislamu wa Shia Ismaili na Mwanzilishi wa Taasisi za Aga Khan, Amefariki Dunia Akiwa na Miaka 88
Aga Khan, kiongozi wa 49 wa urithi wa Waislamu wa Shia Ismaili na mwanzilishi wa taasisi za Aga Khan, ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 88.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (Aga Khan Development Network), alifariki dunia usiku wa kuamkia leo jijini Lisbon, Ureno, akiwa amezungukwa na familia yake.
Mbali na jukumu lake la kiroho, Aga Khan alikuwa mfadhili mashuhuri na mmoja wa viongozi wakuu wa maendeleo ya kimataifa.
Hapa Kenya na kote barani Afrika, alianzisha taasisi kama Hospitali na Chuo Kikuu cha Aga Khan, Nation Media Group, hoteli za Serena, pamoja na miradi mingine mingi ya maendeleo inayotoa ajira kwa maelfu ya watu.
Mchango wake ulienea katika sekta za afya, elimu, na maendeleo ya kiuchumi, si tu barani Afrika bali pia duniani kote.
Aga Khan IV, raia wa Uingereza, alikuwa kiongozi wa kiroho wa jamii ya Waislamu wa Ismaili, inayokadiriwa kuwa na wafuasi milioni 15 duniani kote.
Alirithi wadhifa huo kutoka kwa babu yake mwaka wa 1957 akiwa na umri wa miaka 20 pekee na aliheshimiwa na wafuasi wake kama “mleta uzima.”