
Kamanda wa Kituo cha Polisi cha Nairobi Central, Samson Talam, amefikishwa katika Mahakama ya Milimani kuhusiana na uchunguzi wa mauaji ya mwanablogu na mwalimu wa zamani, Albert Ojwang’. Kufikishwa kwake mahakamani kunajiri siku chache baada ya Mkuu wa DCI, Mohammed Amin, kumtaja kama mshukiwa mkuu katika kifo hicho kilichozua hisia kali.
Mamlaka ya Kusimamia Utendakazi wa Polisi (IPOA) imewasilisha ombi la dharura ikiomba Talam azuiliwe kwa siku 21 katika Kituo cha Polisi cha Lang’ata au kituo kingine chochote nchini, ili kutoa nafasi kwa uchunguzi wa kina kukamilika.
IPOA pia imeitaka mahakama kutoa idhini ya vifaa vya kielektroniki vilivyokamatwa kutoka kwa afisa huyo kufanyiwa uchunguzi wa kitaalamu wa kidijitali, ili kubaini ukweli kuhusu mauaji hayo yanayoendelea kuchunguzwa.