Polisi na maafisa wa afya ya umma walivamia makazi ya mfanyabiashara mmoja wa buchari katika eneo la Makutano, Kaunti ya Embu, ambapo walipata punda 31 waliokuwa wakidaiwa kuibwa, hali iliyozua hofu kwamba huenda wakazi wamekuwa wakila nyama ya punda bila kufahamu.
Kwa mujibu wa mashuhuda, operesheni hiyo ilifanyika Jumamosi baada ya taarifa kutoka kwa umma, zikieleza kuwa eneo hilo lilikuwa likitumika kama kituo cha kuchinja punda kwa ajili ya biashara ya nyama. Walipofika, maafisa hao walipata punda wakichinjwa na nyama ikiwa tayari kusafirishwa.
“Nilishangaa kuona idadi kubwa ya punda waliokuwa wamechinjwa, na ni dhahiri kuwa nyama yao imekuwa ikiuzwa kwa muda,” alisema mkazi mmoja, Josphat Maina.
Milka Ndung’u, mkazi mwingine, alisema kuwa walihesabu vichwa 31 vya punda vilivyotapakaa ndani ya boma hilo.
Hata hivyo, mmiliki wa boma hilo pamoja na wafanyakazi wake walifanikiwa kutoroka wakati wa msako huo. Afisa wa Afya ya Umma wa Mwea, Rachel Nyambura, alithibitisha kuwa nyama hiyo haikuwa imekaguliwa rasmi na hivyo ingetupwa kwa sababu za kiafya.
Kamanda wa Polisi wa Mwea, Willy Simba, alisisitiza kuwa juhudi za kuwasaka wahusika zinaendelea na kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wale wanaojihusisha na biashara hiyo haramu. Wakazi pia walieleza hofu yao kuhusu athari za kiafya zinazoweza kutokana na kula nyama ya punda bila ufahamu.