
Rais William Ruto ametia saini Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Kupambana na Utakatishaji Fedha na Ufadhili wa Ugaidi wa mwaka 2025 kuwa sheria.
Mswada huo, uliopelekwa bungeni na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Kimani Ichung’wah, unalenga kuziba mianya muhimu ambayo imekuwa ikitumiwa kufanikisha utakatishaji wa fedha haramu na mtiririko haramu wa fedha kupitia biashara ya mali na kampuni hewa.
Kupitia sheria hii mpya, jumla ya sheria 10 zimefanyiwa marekebisho ili kushughulikia mapungufu ya kiufundi yaliyobainishwa na Kikundi cha Kupambana na Utakatishaji Fedha cha Afrika Mashariki na Kusini (ESAAMLG), pamoja na Kikosi Kazi cha Kimataifa cha Kupambana na Utakatishaji Fedha (FATF), hasa katika maeneo ya kudhibiti utakatishaji fedha, ufadhili wa ugaidi na usambazaji wa silaha haramu.