
Rais William Ruto siku ya Jumapili alilaani vikali upinzani, akiwashtumu viongozi wake kwa kukosa mpangilio, kuwa na hasira, na kushughulika tu na nia ya kumng’oa mamlakani bila kutoa suluhisho lolote la maana kwa matatizo yanayokumba nchi.
Akizungumza katika Shule ya Kivaywa Comprehensive, Lugari, Kaunti ya Kakamega, Rais Ruto aliwataja viongozi wa upinzani akiwemo Rigathi Gachagua, Kalonzo Musyoka, Eugene Wamalwa, Fred Matiang’i, na Martha Karua, akisema hawana ajenda ya kitaifa ya maendeleo.
“Ujumbe wao pekee ni ‘Ruto lazima aende’. Lakini je, hiyo inatatua matatizo ya afya, elimu au kilimo? Wamejaa hasira na chuki, lakini hawana mpango wowote. Hatutakabidhi uongozi kwa watu kama hao,” alisema Rais Ruto.
Alisisitiza kuwa ataendelea kutekeleza ahadi za maendeleo alizoweka kwa Wakenya, na kuwaonya wanaopinga jitihada hizo kuwa watachukuliwa hatua kali.
Rais pia aliahidi kufufua miradi ya miundombinu iliyo kwama katika Kaunti ya Kakamega, ikiwemo barabara, maji, na umeme, akilaumu mipango mibovu ya awali kwa kuchelewesha utekelezaji wake.
Hata hivyo, Rais Ruto hakugusia mauaji ya hivi majuzi ya mwanablogu na mwalimu wa zamani Albert Ojwang’, kifo ambacho kimezua ghadhabu kubwa miongoni mwa wananchi.
Viongozi wa eneo hilo, wakiwemo Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja, Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa, Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya na Maseneta Boni Khalwale na Godfrey Osotsi, walimtaka Rais kutoa kauli na kuhakikisha haki inapatikana.
Gavana Sakaja alilaani vikali mauaji ya Ojwang’ ambayo yanadaiwa kufanywa na maafisa wa polisi, na kufichua kuwa amempa mjane wa marehemu kazi jijini Nairobi na kununua ardhi kwa ajili ya familia hiyo huko Homa Bay.
“Lakini pamoja na haya yote, hatuwezi kumrudisha. Haki itendeke. Hakuna mtu anayefaa kulindwa,” alisema Sakaja, akionya dhidi ya jaribio lolote la kuficha ukweli.
Kwa upande wake, Gavana Barasa alishangaa ni kwa nini Naibu Mkuu wa Polisi Eliud Lagat, ambaye alikuwa mlalamishi katika kesi iliyompelekea Ojwang’ kukamatwa, bado hajakamatwa.
“Rais, naamini huna watu wa kulindwa. Wote waliohusika wachukuliwe hatua za kisheria,” alisisitiza.
Mbunge Salasya alitaka majibu kuhusu maafisa watatu wa polisi waliompeleka Ojwang’ katika Hospitali ya Mbagathi, na kushangaa kwa nini hawajakamatwa hadi sasa.
Wakati huo huo, Bw. Gachagua alisema kuwa upinzani umeungana na una nia ya kusimamisha mgombea mmoja katika uchaguzi wa 2027 kumkabili Rais Ruto.
“Rais Ruto anajaribu kutugawanya, lakini hatutakubali. Tuko tayari na tutaibuka na ushindi. Tunatoa wito kwa Wakenya wote kuungana nasi kumng’oa Dkt. Ruto,” alisema Gachagua.
Kwa upande mwingine, Muungano wa Makanisa ya Kenya ulilaani mauaji ya Ojwang’, yakilitaja kama fedheha kubwa kwa maadili ya Huduma ya Polisi nchini.
Akipiga ziara ya rambirambi kwa familia ya marehemu, Makamu Mwenyekiti wa muungano huo, Askofu Stephen Mutua, alitoa wito kwa Mamlaka ya Kusimamia Polisi (IPOA) kuharakisha uchunguzi wa kifo cha Ojwang’ pamoja na vifo vingine vya vijana ambavyo havijapatiwa majibu.
“Tunataka sio tu kesi hii ichunguzwe, bali pia vifo vyote vya vijana ambavyo bado havijapatiwa ufumbuzi, na wahusika wafikishwe mbele ya sheria,” alisema Askofu Mutua.
Aliitaka pia Idara ya Polisi chini ya Mkuu wa Polisi Douglas Kanja kuhakikisha kuwa maandamano ya amani yanaheshimiwa, huku akionya waandamanaji kuepuka vurugu zinazoweza kuleta maafa zaidi.
“Vijana wa Kenya, elezeni kilio chenu kwa njia ya amani na kwa kuzingatia sheria. Huo ndio msingi wa kulinda haki yetu ya maandamano na kuepusha upotevu wa maisha,” alisema.
Muungano huo ulitoa wito kwa Rais Ruto kuongoza juhudi za kurejesha imani ya umma kwa vyombo vya usalama, na kuanzisha mageuzi yatakayowiana na maadili ya kikatiba.