
Mwanamuziki wa nyimbo za Mugithi, Samuel Muchoki almaarufu Samidoh, anazidi kuibua sintofahamu baada ya kutoripoti kazini katika Kikosi Maalum cha Kukabiliana na Wizi wa Mifugo (ASTU) licha ya agizo rasmi la Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS).
Kulingana na barua ya ndani ya polisi iliyosainiwa na Kennedy Barasa kwa niaba ya Kamanda wa ASTU, Joseph Limo, Samidoh alitakiwa kurejea kazini mnamo Mei 27, 2025, baada ya kumaliza likizo aliyokuwa amepewa. Hata hivyo, tangu tarehe hiyo, hajawahi kurudi kazini wala kutoa maelezo yoyote kuhusu kutokuwepo kwake, jambo ambalo limewafanya wakubwa wake kumtangaza rasmi kama afisa aliyehepa kazi (deserter).
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mshahara wa Samidoh umesitishwa mara moja na polisi katika Kaunti ya Nyandarua waliagizwa kufuatilia nyumbani kwake ili kupata taarifa za aliko.
Kabla ya tukio hilo, Samidoh alikuwa amehamishiwa kutoka kikosi chake cha awali kufuatia tukio la moja ya maonyesho yake ambapo mashabiki walikuwa wakiimba kauli tata ya kisiasa, jambo lililozua mjadala ndani ya jeshi la polisi.
Kwa upande mwingine, msanii huyo amekuwa akionyesha dalili za kutofautiana na agizo hilo la kurudi kazini, hasa baada ya kuchapisha ratiba ya maonyesho yake ya kimataifa nchini Marekani kupitia mitandao ya kijamii. Kwenye chapisho hilo, Samidoh aliorodhesha miji kama Houston, Texas, Massachusetts, Dallas na Washington kama maeneo atakayotumbuiza kati ya Juni na Julai. Aliambatanisha ratiba hiyo na methali ya mafumbo: “Hata tai huruka juu angani, huteremka kutafuta chakula. Methali ya wenye hekima.”
Hata hivyo, nyaraka nyingine zilizovuja kutoka kwa NPS zinaonyesha kuwa Aprili 25, 2025, Samidoh alipewa ruhusa rasmi ya kusafiri kwenda Marekani kuanzia Mei 20 hadi Juni 9, hali inayotia dosari hatua ya kumtangaza kuwa ametoroka kazi kabla ya muda wa likizo kumalizika.
Kisa hiki kinaibua maswali kuhusu mawasiliano ya ndani ya taasisi za usalama na jinsi ya kushughulikia maafisa wa umma wanaojihusisha na taaluma mbili zenye mgongano wa kisheria au kimaadili.