Serikali Yasema Hakuna Nafuu ya Ushuru Hivi Karibuni
Wakenya wataendelea kubeba mzigo wa ushuru kwa muda zaidi, kwani serikali bado haijafanikisha malengo yake ya ukusanyaji mapato.
Waziri wa Fedha, John Mbadi, alieleza kuwa viwango vya Ushuru wa Mshahara (PAYE) na Ushuru wa Ongezeko la Thamani (VAT) haviwezi kupunguzwa hadi Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Kenya (KRA) ifanikishe lengo lake la mapato kwa muda wa angalau miezi sita mfululizo.
“Ikiwa tungeweza kupunguza ushuru, ingekuwa afueni kwa wananchi. Hata hivyo, kwa sasa tunakabiliana na mzigo wa madeni, hivyo basi kupunguza ushuru kutapunguza mapato ya serikali, jambo ambalo haliwezekani kwa sasa,” alisema Mbadi katika mahojiano na NTV kwenye kipindi cha Fixing The Nation.
Kauli hii inakinzana na ahadi aliyotoa Agosti mwaka jana aliposema kuwa serikali ingeweza kupunguza VAT kutoka asilimia 16 hadi 14, pamoja na PAYE na Ushuru wa Kampuni.
Mnamo Septemba 9, 2024, wakati wa uzinduzi wa mchakato wa bajeti ya mwaka wa kifedha 2025/2026, Mbadi alidokeza kuwa kupunguza viwango vya ushuru kungesaidia kukuza uchumi wa taifa.
Hata hivyo, Waziri huyo sasa anasisitiza kuwa hakuna mpango wa kuongeza au kuanzisha ushuru mpya ambao unaweza kuwa mzigo kwa wananchi.
Kuhusu hatua za kuwapunguzia wananchi mzigo wa kifedha, alisema kuwa tayari serikali imepunguza makato ya bima ya SHA na Ushuru wa Nyumba kwa asilimia 30 baada ya kupitishwa kwa Sheria ya Ushuru Desemba mwaka jana.