
Maelfu ya vijana waliingia mitaani katika maeneo mbalimbali ya jiji la Nairobi Jumanne wakitaka kujiuzulu kwa Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Eliud Lagat, wakihusisha afisi yake na kifo cha mwanablogu Albert Ojwang’.
Maandamano hayo yaliibua hali ya taharuki jijini huku shughuli nyingi zikiathirika, hasa wakati ambapo nchi inasubiri hotuba ya bajeti ya mwaka wa kifedha 2025/2026 kutoka kwa Waziri wa Fedha, John Mbadi.
Waandamanaji walionekana wakielekea maeneo ya jiji kuu, wakipitia barabara muhimu kama vile Harambee Avenue, huku wakizuiwa kwa vitoa machozi na polisi waliowekwa kulinda majengo ya serikali ikiwemo Bunge la Kitaifa. Kundi hilo pia liliimba nyimbo za upinzani na kauli maarufu ya “Wantam” huku wengine wakivalia nguo zenye rangi za bendera ya taifa.
Polisi waliimarisha doria na kufunga baadhi ya barabara, wakiweka vizuizi na kufanya ukaguzi mkali hasa kwenye barabara ya Thika, juhudi ambazo zilionekana kama njia ya kudhibiti wingi wa watu wanaoingia katikati mwa jiji.
Kutokana na hali ya sintofahamu, baadhi ya wafanyabiashara walilazimika kufunga maduka yao kwa hofu ya uvunjaji wa amani na uporaji.
Maandamano haya yanajiri wakati viongozi waandamizi wa polisi wakiongozwa na Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja na Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) Mohamed Amin wakitoa ushahidi mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu kifo cha Ojwang’, tukio ambalo limezua hisia kali kitaifa.